LINAH AFUNGUKA JUU YA STAR ALIYEMTAKA KUSAGANA
Posted in
No comments
Wednesday, April 9, 2014 By Unknown
Makala: Joseph Shaluwa
NIKISEMA msichana huyu ni kati ya mastaa wa Bongo Fleva wanaofanya vizuri nitakuwa sijampa sifa za bure! Ni kweli anaweza. Sauti yake, anavyoweza kutawala jukwaa ni kati ya mambo yanayosherehesha sifa hiyo.
Ni msichana mdogo tu, mzaliwa wa tatu kati ya watano kutoka familia ya mzee Peter Sanga. Jina lake halisi ni Estelina lakini maarufu zaidi kwa jina la Linah akiwa zao la Nyumba ya Vipaji Maalum Tanzania ‘THT’.
Kibao cha Atatamani ndicho kilichomtambulisha kwenye ramani ya muziki mwaka 2009, leo miaka mitano baadaye, tayari Linah ni gumzo kwenye ulimwengu wa muziki. Achilia mbali kazi zake kisanii, kutokana na umaarufu wake, maisha yake binafsi yamegeuka kuwa habari.
Hapa kwenye Exclusive Interview, Linah ameeleza mambo mengi yanayohusu maisha yake nje na ndani ya sanaa. Kwanza nilimwulizwa kuhusu madai ya kuandikiwa nyimbo zake. Hapa anajibu bila wasiwasi: “Hilo siwezi kubisha, unajua kila mtu ana kipaji chake, mimi naweza zaidi kuimba. Nyimbo nyingi nimeandikiwa na Amini (Mwinyimkuu) na Barnaba (Elius).”
Inasemekana bado una uhusiano na Amini, ikoje?
Mh! Nadhani watu wanashindwa kuelewa. Kweli Amini alikuwa mpenzi wangu, tena tulioshibana na kufikia hatua ya mbali kabisa lakini tumeachana.
Hata hivyo, kutokana na kazi zetu, huwa tunakutana mara kwa mara, naonekana naye mahali popote, labda ndiyo maana watu wanafikiri bado tunaendelea.
Mimi nina mtu wangu na kila mtu anamjua – Nagari Kombo (yule aliyemkumbatia mchezaji wa Timu ya Taifa ya Brazil, Ricardo Kaka, Uwanja wa Taifa) na Amini naye ana maisha yake.
Nini kiliwatenganisha?
Hakuna kitu cha moja kwa moja ambacho naweza kukitaja kuwa ni sababu ya kuachana kwetu. Nilimpenda sana Amini, naye alinipenda pia, lakini kuna mambo tulikuwa hatuendi sawa.
Ilifikia mahali tukaona kwa namna hali ilivyokuwa, hatuwezi kuendelea kuwa wapenzi. Tukaamua kuachana ingawa lazima nikiri kuwa tuliachana tukiwa bado tunapendana.
Unatajwa kwenye usagaji, ni kweli?
Usagaji upo sana kwa mastaa, nausikiasikia lakini mimi sijawahi kusagana na wala sifikirii. Lakini ni kweli kuna staa mmoja, naomba nisimtaje, alianza kuonyesha dalili za kunitaka kwenye huo mchezo mchafu, nikavunja urafiki naye.
Vipi bifu lako na Jaydee?
Aisee katika wanamuziki wa kike wanaonivutia, Jide (Judith Wambura) ni wa kwanza. Ni kweli kulitokea kutokuelewana kati yetu, ni mambo ya kawaida kwenye kazi. Natamani sana siku moja nifanye naye kazi.
Unajifunza nini kupitia Ray C?
Ray C (Rehema Chalamila) ni mzuri, anaimba vizuri, ana mwonekano mzuri na anajua anachokifanya kwenye game. Mambo yaliyopita hapo kati naweza kusema ni ajali tu, lakini uzuri ni kwamba ameshaachana na hayo mambo (matumizi ya madawa ya kulevya).
Inawezekana aliingia kwa kujaribu au kuwaiga mastaa wenye mchezo huo, lakini matokeo yake yamekuwa tofauti. Nashauri wasanii wenzangu, tuwe makini, siyo kila kitu cha kuiga.
Nini kinaendelea kati yako na Mchungaji Gwajima?
Mchungaji Josephat Gwajima (wa Kanisa la Ufufuo na Uzima) ni baba yangu wa kiroho. Alinisaidia sana. Kuna wakati nikiwa nasoma, nilisumbuliwa sana na mapepo. Wazazi wangu walihangaika sana na mimi, baadaye wakanipeleka kanisani kwake.
Niliishi pale karibu mwaka mzima. Ilibidi nihairishe mwaka mmoja wa kidato cha tatu. Ilikuwa maombi muda wote. Nashukuru Mungu nilipona na nikafanikiwa kumaliza masomo yangu. Mpaka sasa naendelea vizuri.
Mafanikio yako kimuziki yakoje?
Nashukuru muziki umenisaidia mengi. Kwanza najulikana, napata dili kila kukicha. Kuna nyumba ya familia tunajenga Mbezi, kuna biashara zangu nipo mbioni kufungua na naihudumia familia yangu vizuri.
Siishi kwetu, nimepanga nyumba yangu mwenyewe na ninajilipia kodi, naweza kujihudumia kwa kila kitu! Kwangu hayo ni mafanikio, mengine yatakuja taratibu.
Kwanini umesisitiza unajilipia kodi mwenyewe?
(Anacheka) Mh! Unajua wasichana wengi wa mjini wanalipiwa nyumba na mabwana zao, ndiyo maana mimi naona ni heshima kufanya hivyo mwenyewe na kuliweka wazi.
Mahojiano haya yanapatikana Global TV Online iliyo ndani ya mtandao namba moja wa burudani Bongo, www.globalpublishers.info ambapo utakutana na mastaa wengine kibao.
Related posts
Share this post
0 comments: