KILIMANJARO, TANGA, ZAONYESHA DALILI ZA MAFUTA, URANI
Posted in
No comments
Tuesday, December 31, 2013 By Unknown
KWA UFUPI:
Profesa Maghembe alisema taarifa za wataalamu wa miamba pia zinaonyesha kugunduliwa kwa madini ya Urani katika milima ya Kijiji cha Kivisini.
Moshi. Mikoa ya Kilimanjaro na Tanga, imeonyesha kuwa na matumani ya kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta.
Mkoa wa Kilimanjaro pia umeonekana kuwa na dalili za kuwa na madini ya urani na kuufanya mkoa huo wenye mlima mrefu kuliko yote Afrika, kuwa na uwezekano wa kuwa na utajiri wenye manufaa makubwa kwa Tanzania.
Wakuu wa mikoa hiyo, jana walithibitisha kuwa tafiti zilizofanyika kwa nyakati tofauti, zimethibitisha matumaini ya utajiri huo.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama alisema katika mkoa wake mafuta yamegundulika katika Bonde Pangani katika vijiji vya wilaya za Moshi Vijijini, Mwanga na Same.
“Ni kweli kuna watu wanafanya utafiti wa mafuta pale Chekereni Moshi Vijijini kuna mwelekeo wa kupatikana kwa mfuta katika bonde lote hilo kuanzia Same hadi Moshi Vijijini,” alisema Gama.
Gama alisema ishara za kuwepo kwa mafuta ndizo zilizosukuma kuanza kwa utafiti huo.
“Tusubiri tuone yakipatikana itakuwa ni neema kwa Kilimanjaro na taifa,” alisema.
Wakati mkuu wa mkoa akisema hivyo, Mbunge wa Mwanga ambaye pia ni Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, naye alithibitisha kuwepo kwa dalili za kupatikana kwa mafuta katika ukanda huo.
“Ni kweli walianzia utafiti wao pale Ziwa Chala na Ziwa Jipe halafu wakaenda hadi Kijiji cha Butu mpaka Mkomazi pale jimboni kwangu na kuna dalili za kuwapo kwa mafuta,” alisema Profesa Maghembe.
Profesa Maghembe alisema taarifa za wataalamu wa miamba pia zinaonyesha kugunduliwa kwa madini ya Urani katika milima ya Kijiji cha Kivisini.
“Hii ni neema kwa kweli kwa sababu rasilimali zote hizi mbili zikigunduliwa hapa kwetu ni manufaa makubwa ya kiuchumi si kwa mkoa tu lakini kwa taifa zima hili si jambo dogo,” alisema waziri.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa alisema dalili za kuwepo kwa mafuta katika ukanda wa bahari ya mkoa wake, zimeanza kuonyesha matumaini na utafiti kwamba unatarajia kukamilika mwaka ujao.
Habari: Mwananchi
Related posts
Share this post
0 comments: