LISSU: WALIPOTELEA WAPI WAASISI WA MUUNGANO
Posted in
No comments
Tuesday, May 13, 2014 By Unknown
Serikali imetakiwa kutoa maelezo bungeni, kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wanaodaiwa kuzikwa katika handaki moja Zanzibar.
Akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), msemaji wake, Tundu Lissu aliitaka Serikali kueleza waasisi hao walifanya makosa gani.
Aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdallah Kassim Hanga aliyekuwa Waziri Mkuu, Abdulaziz Twala aliyekuwa Waziri wa Fedha na Saleh Akida aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi, Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema waliuawa na kuzikwa handaki moja eneo la Kama, Zanzibar.
Lissu alisema hayo huku akinukuu kitabu cha 'Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru' kilichoandikwa na Harith Ghassany alichosema kilionyesha jinsi viongozi hao walivyouawa na kuzikwa katika kaburi moja.
"Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa katika kaburi au handaki moja," alisema Lissu huku wabunge wakiwa kimya kumsikiliza.(P.T)
Mgawo wa Zanzibar
Lissu pia aliibua mambo mazito kuhusu mgawanyo wa fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Alisema Muungano ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji ambao nchi kubwa imeifanyia nchi ndogo ya Zanzibar kwa miaka mingi.
Alikwenda mbali na kuitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au Wazanzibari kwa umoja wao, kufungua kesi Mahakama za kimataifa kudai fedha zote ambazo nchi yao imeibiwa kwa kivuli cha Muungano.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alisema hadi Machi mwaka huu, Zanzibar ilikuwa imepata gawio la Sh27.1 bilioni badala ya Sh32.6 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge, sawa na asilimia 83.
Hata hivyo, alisema hilo linaweza lisiwe tatizo, kwani kwa mwelekeo wa takwimu hizo, hadi kufikia mwisho wa mwaka huu wa fedha, gawio lililoidhinishwa linaweza kuwa limelipwa lote.
Haya hivyo, alisema tatizo kubwa na la msingi ni kwamba, gawio lililoidhinishwa na Bunge si halali kwa Zanzibar, kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya ya Aprili 30, mwaka huu.
Chanzo: www.mwananchi.co.tz
Related posts
Share this post
0 comments: